*Shida isikutoe kwenye mstari*
Wimbo wa *Ni Salama Rohoni Mwangu* ulitokana na mikasa iliyomkuta mwanasheria na wakili mahiri mkristo aliyeitwa Heratio Spafford.
Alikuwa na watoto watano akiwemo wa kiume mmoja. Mwanae pekee wa kiume alifariki mwaka 1871 akiwa na miaka minne.
Mwaka 1872 kulizuka moto mkubwa sana maarufu kama moto mkubwa wa Chicago ambao uliteketeza shamba na majumba yake, vitu alivyokuwa amejipatia kwa fedha alizoingiza kutokana na umahiri wake katika taaluma na kazi yake.
Mwaka 1873 alitanguliza mkewe na mabinti zake wanne kwenda mapumziko Ulaya ambapo angewafuata kesho yake baada ya kumaliza kazi alizokuwa nazo.
Meli iliyokuwa ikiitwa Ss Ville du Havre iliyobeba familia yake ilizama na binti zake wote walifariki akapona mkewe tu ambaye alimtumia telegramu *Nimepona mimi tu*.
Akiwa njiani kurudi nyumbani kwake nyumba ilimokuwa ofisi yake ikaungua. Kwa bahati nzuri nzuri alikuwa ameikatia bima lakini kampuni ya bima ilikataa kumlipa kwa madai kuwa lile lilikuwa janga la asili (An Act of God). Heratio alibaki mtupu - hana pa kuishi wala hana fedha. Akiwa ni mtu wa kiroho aliyemtegemea Mungu alikaa akitafakari yale yaliyokuwa yakitokea katika maisha yake na ndipo alipochukua kalamu na karatasi na kuandika *"Lolote liwalo, Bwana wangu, umenifundisha kusema - Ni salama rohoni mwangu*". (Maandishi mengine yanasema aliandika maneno haya alipofika eneo la bahari ilipozama meli akiwa safarini kumfuata mkewe Ulaya). Baadae maneno haya yaliongezwa mashairi na kutiwa muziki na kuwa wimbo maarufu sana na wenye mguso wa kipekee wa *Salama Rohoni*. Kama ilivyokuwa kwa Ayubu Heratio alikuja kuinuliwa akapata watoto wengine na mali na fedha.
Mpendwa uliyefiwa, unayeuguza, unayeugua, uliyeishiwa, uliyevunjwa moyo, unayepitia tabu yoyote tukumbuke hakuna giza la kudumu. Tukumbuke Mungu yupo na ameahidi kumlinda kila amtazamaye asivunjwevunjwe au kufa moyo kutokana na taabu.
Kwa mfano huu wa Heratio tunajifunza kuwa ukubwa wa jaribu si tatizo bali mitazamo yetu kuhusu maisha. Ukipatwa na shida ufanye nini? Ujione hufai? Useme Mungu amekuacha? Useme shetani amekuinukia na amekushinda? Ujitoe uhai? Ulalame na kunung'unika usiku na mchana siku nenda rudi? La hasha! Kwanza ondoa tumaini lako kwenye vitu vya kupita na uweke tumaini lako kwa Mungu aliyeviumba na kukuumba. Nafsi yako imhimidi Mungu na kumshukuru kwani pamoja na shida yako kuwa nzito bado kuna vingi vya kumshukuru kwavyo. Hata hivyo atabaki kuwa Mungu. Huyu Mungu amesema katika mambo yote anakuwazia mema. Hata katika jambo baya kwako kuna jema analokuwazia ambalo wewe hulioni. Daudi alisema ajapopita katika bonde la uvuli wa mauti (shida, mateso, majaribu) hataogopa mabaya kwani anaamini katika gongo na fimbo ya Mungu. Akazidi kusema anataka neno moja tu kwa Bwana, nalo ndilo atakalolitafuta. Autazame uzuri wa Bwana na kutafakari hekaluni mwake. Hekaluni mwa Bwana ni kwenye moyo wako. Tafakari ukuu wa Mungu humo badala ya ukuu wa tatizo.
Iwe salama, salama moyoni mwako. Amen.
No comments:
Post a Comment