Sunday, March 5, 2017

TEMBEA NURUNI MWA KRISTO

Shalom Kanisa
Biblia inasema  "bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. (1 YOH. 1:7 SUV).*
Moja ya vitu ambavyo shetani atavihakikisha pale unapokuwa na majanga ni kukukata na ushirika na watu wengine wa Mungu.
Atakufanya ujisikie vibaya mpaka uone kuwa hustahili kuwa katika ushirika na watu wengine wa Mungu.
Ataweka uzito kwako wa kuhudhuria katika ushirika na watu wengine wa Mungu.
Atafanya hivyo maana anajua nguvu ya ajabu ya ushirika.
Anajua walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa Jina Lake Yeye huwa Naye anakuwepo hapo katikati yao.
Anajua mahali Alipo Bwana Damu Yake pia ipo kuwatakasa watu na dhambi yote.
Anajua kuja kwako tu katika ushirika na wapendwa wenzio kuna Damu ipo itakayokutakasa na dhambi yote.
Anajua kuwa moja ya vitu vilivyopo Sayuni yaani katika kusanyiko la wateule ni Damu ya kunyunyizwa ya Mwana Kondoo wa Mungu ituneneayo mema kuliko ile ya Habili.
Shetani anapokuwekea uzito wa kufika kusanyikoni au kanisani au kwenye ushirika na wapendwa wengine ndo hilo analilenga.
Hataki ukutane na Damu ya Yesu itakasayo.
Hataki ukutane na Damu ya Yesu ikuneneayo mema.
*Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji. Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu. (ZEK. 9:11-12 SUV).*
Anajua kabisa kuwa hio Damu ya Agano ya Mwana Kondoo itakutoa kwenye shimo lisilo na maji.
Mashimo yasiyo na maji yalikuwa yanatumika kama magereza katika siku za kuandikwa huu mstari.
Kwa hiyo kimsingi shetani atakukata na ushirika ili Damu ya Yesu isikutoe katika magereza mbali mbali ambayo umo iwe ya kitabia, ya kimwenendo, na ya aina mbalimbali.
Anatuambia tuikimbilie ngome.
Ngome ipi?
Ngome ya Damu ya Yesu ambayo inakuwa dhahiri sana kwenye ushirika wa watu wa Mungu.
Tena anawasemesha wafungwa wa tumaini.
Yaani hata kama umefungwa leo alimradi huachi kuja ushirikani, ibadani, kwenye kusanyiko la watu wa Mungu lipo tumaini kwa ajili yako.
Damu ya Yesu itakutoa kwenye hicho kifungo.
Ndiyo maana tunasisitizwa tusiache kukusanyika.
*wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia. (EBR. 10:25 SUV).*
Anajua ukikusanyika utapokea maonyo toka katika Neno la Mungu.
Anajua nguvu ya maonyo kulainisha moyo wa mwanadamu.
*“Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.” (EBR. 3:13 SUV).*
Anajua kuwa ukiendelea kuja nyumbani mwa Bwana kukusanyika na wapendwa wenzio utapata maonyo kupitia neno linalohubiriwa na kufundishwa ili moyo wako usije ukafanywa mgumu na udanganyifu wa dhambi.
Na ndo hilo shetani hataki kwa hiyo anakuhubiria na kukupa sababu kwanini usiende Nyumbani Mwa Bwana.
Anakuambia wewe kaa tu nyumbani.
Anakuambia wewe ingia mtaa.
Anakuambia kwanza wewe hufai wala hustahili.
Kumbe ni kampeni zake za kukuweka mbali na Damu ya Yesu ijidhihirishayo kusanyikoni na Neno la Mungu la maonyo kwako.
Kuna wengine mtakuwa mnasoma hii ambao mmekata tamaa hata kumtumikia Mungu kwa ajili ya kile kinachoendelea maishani mwenu.
Unajisikia hatia.
Unajisikia hukumu.
Sikia mpendwa wangu.
Mungu hawatumii wakamilifu bali anawakamilisha anaowatumia.
*“Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.” (YN. 15:2 SUV).*
Shetani anakufosi kukutoa katika utumishi ili usimzalie Bwana matunda ili hatimaye kama tawi uondolewe kwenye mzabibu na kutupwa nje.
Anajua alimradi yapo matunda unamzalia Bwana basi Bwana ataendelea kukusafiaha na kukutakasa ili umzalie matunda zaidi.
Akusafishe na nini sasa kama wewe ni mkamilifu?
Anakusafisha na mapungufu maishani mwako.
Hakusafishi kwanza ndipo akutumie bali anakusafisha huku anakutumia.
Sasa shetani anakumezesha uongo kuwa utamtumikiaje Mungu hivyo na wewe unaumeza uongo wake unaacha na kujikata mwenyewe toka kwenye mzabibu na kujiondoa mwenyewe kwenye mchakato wa kusafishwa na kutakaswa ili uweze kuzaa zaidi.
Tunapoelekea Mwaka Mpya nasema hivi ewe uliye mbali na ushirika na watu wa Mungu rejea katika ushirika na wewe mtumishi ambaye umeamua kuweka silaha chini zinyanyue tena rudi shambani ili Mungu awe na sababu ya kukusafisha maana unamzalia matunda.
Ni kweli Mungu ni moto ulao na madhabahu Yake ina Moto Wake.
Sasa ukikaa mbali na hiyo madhabahu hivyo vitu vitaondolewa vipi maishani mwako na moto wa Mungu?
Weka maisha yako tena madhabahuni kwa Bwana ili moto Wake uunguze na kuteketeza kila kisicho Yeye maishani mwako.

No comments:

Post a Comment