Wednesday, January 25, 2017

6Ngoja nikuonyeshe kitu kingine. Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. (GAL. 5: 16 - 17). Maandiko hapa yapo wazi kuwa tukienenda kwa Roho hatutatimiza kamwe tamaa za mwili. Unapokoka tamaa za mwili hazifi. Ila unazidhibiti kwa kuenenda kwa Roho. Huwezi kuenenda kwa Roho kama roho yako wewe ni dhaifu. Kinachofanya roho yako iwe na nguvu ni kuukulia kwako wokovu na kuukulia kwako wokovu kunategema mafundisho sahihi unayopata na jitihada binafsi za kinidhamu za usomaji wa neno. Wengi wanahangaika na kutimiza tamaa za miili yao kwa sababu hawaenendi kwa Roho na wanashindwa kuenenda kwa Roho kwa sababu roho zao ni dhaifu na ni dhaifu kwa sababu hawajaukulia wokovu na hawajaukulia wokovu kwa sababu hawajayatamani maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ambayo ni mafundisho sahihi ya neno la Mungu na usomaji binafsi wa neno la Mungu. Kukua ndiko kunakoongeza nguvu ya roho zetu na kurahisisha kuenenda kwetu kwa Roho. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli. (LK. 1: 80). Kwa kadiri unavyokua ndivyo unavyoongezeka nguvu rohoni na inakuwa rahisi kuyaishi maisha ya kuenenda kwa Roho maana roho iliyokua ni rahisi sana kumwitikia Roho Mtakatifu. Ngoja nikuonyeshe andiko lingine: mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. (EFE. 4:22 - 24). Katika andiko ambalo tumetoka kunukuu tunaambiwa tuvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani unaoharibika kwa kufuata tamaa zenye kudanganya. Kuvua ni mchakato ambao unawezeshwa na kufanywa upya roho ya nia zetu kwa njia ya mafundisho sahihi ya neno la Mungu na usomaji wa neno katika maisha ya mwamini. Hatuishii tu kwenye kuuvua utu wa zamani bali pia tunaenda hatua moja zaidi ya kumvaa mtu mpya aliyeumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. Huu mchakato wa kuuvua utu wa zamani na kuuvaa utu mpya ndo unaitwa kuongoka na unawezekana tu kama tayari umeokoka. Lakini pia tuwe makini kujua kuwa kuongoka hakutokei tu kwa sababu umeokoka. Kuongoka kunatokea kwa sababu kuna hatua za makusudi unazichukua kama ambavyo tumeona kwa sehemu kwenye hili somo la leo. Tuangalie tena andiko lingine. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. (EFE. 4:15). Kwa kadiri tunavyoishika kweli (ambayo ni neno la Mungu, na hiyo twaishika kwa kuiishi, huku tukisukumwa na upendo wetu kwa ajili ya Bwana), tunakua hata kumfikia Yeye Yesu katika yote kimwenendo na kitabia. Huku sasa ndo kuongoka. Nimalizie somo la leo kwa andiko lingine. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho. (2 KOR. 3: 18). Uso usiotiwa utaji unaozungumziwa kwenye andiko tulilonukuu ni uso ambao haujazibwa kuona kile ambacho neno la Mungu linatufundisha. Kwa kadiri tunavyoelewa kile ambacho neno la Mungu linafundisha hilo litaonekana zaidi katika maisha yetu ya kimwenendo na kitabia na itapelekea sisi kubadilishwa ambako ndiko kuongoka kwenyewe. UMEBARIKIWA MNO, YESU AKUTUNZE.

No comments:

Post a Comment