KUOKOKA NA KUONGOKA Bwana Yesu Asifiwe. Neema na Amani zizidishwe kwako. Napenda nizungumze na wewe kidogo. Ukiangalia kwa haraka haraka unaweza ukaona maana ya hivi vitu viwili KUOKOKA na KUONGOKA.vipo sawa lakini havipo sawa hata kidogo. Yesu siku moja akizungumza na wanafunzi Wake aliwaambia: Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. (LK. 22:31, 32). Katika hayo maandiko hapo juu inaonekana wanafunzi wangepitia mahali pagumu lakini Yesu akawa amemwombea Petro ili imani yake isitindike au isishindwe na akamwambia atakapoongoka, au kwa maneno mengine atakapobadilishwa kutoka kwenye hiyo hali kurejea kwenye hali ambayo alitakiwa awe nayo awasaidie wengine. Tunapozungumzia kuokoka tunazungumzia kutolewa dhambini na Yesu kwa njia ya muujiza wa kuzaliwa mara ya pili. Ni kuhamishwa toka kwenye ufalme wa giza kuja kwenye Ufalme wa Mwana wa Pendo Lake. Ni kutoka gizani kuja nuruni. Kuokoka kunazungumzia zaidi kuhamishwa. Kuongoka ni kitu ambacho kinaanza kutokea baada ya kuokoka. Ni badiliko ambalo linaanza na kuendelea ndani ya mtu baada ya kuokoka ili kumfanya azidi kufanana na asili ya uamuzi ambao ameuchukua wa kumpa Yesu maisha Yake. Tuangalie maandiko mawili matatu tuweze kuelewa kidogo hiki kitu. Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. (MT. 11:28 - 30 ). Kwenye mistari ambayo ndo tumetoka kusoma kuna vitu viwili vinazungumziwa kwenye hii mistari. 1. Kuja kwa Yesu ambako ndo kuokoka kwenyewe. 2. Kujifunza kwa Yesu ambako ndiko kutakakosababisha badiliko ambalo ndo kuongoka kwenyewe. Wengi wakishaokoka wanafikiri ndo mwisho wa kila kitu wakati kuokoka ni mwanzo tu wa safari. Baada ya kuokoka lazima ujifunze namna mpya ya kuishi kwa kujifunza maneno ya Mungu. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. (MT. 28:19 - 20 ). Yesu alipowaagiza wanafunzi Wake wakawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi aliwapa vitu viwili vya kufanya: 1. Wakawabatize ambako ndiko kuokoka maana sehemu nyingine maandiko yanasema aaminiye na kubatizwa ataokoka. 2. Kuwafundisha kushika yote aliyo waamuru ambako ndiko kutazaa kuongoka au badiliko la kitabia. Wengi wamefadhaishwa na kukatishwa tamaa na wokovu maana hawaoni badiliko la kitabia baada ya kuokoka wasijue kuwa wokovu huleta badiliko la hadhi (status) na mafundisho ndiyo huleta badiliko la kitabia na mwenendo. Kwa kadiri mtu unavyojitoa kwenye mafundisho na kulisoma neno la Mungu unajengwa kwenye utu wako wa ndani ili uweze kuanza kubadilika kitabia na kimwenendo. Embu tuangalie andiko lingine. Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. (YN. 8:31 - 32). Katika andiko ambalo ndo tumetoka kusoma tena tunaona kuna vitu viwili vinazungumziwa: 1. Kumwamini Yesu ambako ndiko kuokoka. 2. Kuendelea katika neno Lake ambako ndiko kunaleta mabadiliko ya kitabia na kimwenendo ndani ya mtu ambako ndo kuongoka kwenyewe. Wengi wamepitia hatua ya kwanza ya kuokoka lakini kwa sababu hawakuendelea katika neno Lake kwa njia ya mafundisho na usomaji wa neno hawajaanza kuona mabadiliko ya hatua ya pili. Hatuwezi kuwekwa huru kimwenendo na kitabia kama tusipoendelea kwenye hatua ya pili ambayo ni ya kuendelea katika neno Lake. Wengi wamekatishwa tamaa na kutokubadilika kwa tabia zao baada ya kuokoka kwa sababu hakuna hatua za makusudi ambazo wanazichukua kujenga mazingira ya badiliko hilo au wamejenga lakini hawajaipa muda wa kutosha wa kuanza kusababisha hilo badiliko. Kuna kuokoka na kuna kuukulia wokovu. Kuokoka ni tukio ambalo atokana na uamuzi wa kunfanya Yesu Bwana.na Mwokozi wa maisha yetu. Kuukulia wokovu ni mchakato na huo mchakato ndo unaitwa kuongoka. Tuangalie tena andiko lingine. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; (1 Petro 2: 2). Watoto wachanga waliyozaliwa sasa ndo hao waliyookoka na tukishaokoka tunatakiwa kuyatamani maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ambayo ni mafundisho sahihi ya neno la Mungu na usomwaji wa neno. Usipokuwa msomaji wa neno na mhudhuriaji wa mafundsisho huwezi kuukulia wokovu na usipoukulia wokovu huwezi kuona badiliko la kitabia na kimwenendo maishani mwako. Hapo ndo wengi walipokwama.
Kweli kabisa nimejifunza mengi juu ya tofauti hizo, bwana YESU asifiwe!
ReplyDeleteNi lini au ni wakati gani Petro aliongoka? Kwa mafundisho yaliyotolewa na nani?
ReplyDeleteNdugu Kama haukubalihilo inawezekana unasali makanisa ya imani potofu hebu jitathimini dhehebu lako.
Deletenimejifunza
ReplyDeleteJaman jamani Hili Gombo ni Tamu sana.... MUNGU akubariki na kuachilia mafuta ya Roho juu yako yazidi kutufundisha.
ReplyDelete